Return   Facebook   Zip File

Obligatory

Bahá’u’lláh alifunua sala tatu za faradhi, ambazo mojawapo inaweza kuchaguliwa na kila muumini na kuisoma mara moja katika saa 24, kufuatana na maelekezo maalum kwa kila sala. Agizo linalohusiana na sala iliyotolewa hapo chini, ambayo ndiyo fupi kabisa kati ya tatu, ni kwamba ni lazima isemwe mara moja kwa siku kati ya adhuhuri na machweo.

Nashuhudia, Ewe Mungu Wangu, kwamba Wewe Umeniumba, kukujua Wewe na kukuabudu. Nashuhudia katika wakati huu, juu ya unyonge wangu na uwezo Wako, juu ya umaskini wangu na utajiri Wako.

Hakuna Mungu mwingine ila Wewe Msaada katika Mashaka, Aliyepo Mwenyewe.

#11207
- Bahá'u'lláh

 

General

ALFAJIRI

Ee Mungu na Bwana wangu! Mimi ni mutumishi Wako na Mwana wa mtumishi Wako. Nimeamka kutoka kitandani mwangu kwenye mapambazuko haya wakati Nyota ya Mchana ya umoja Wako imemulika kutoka Mapambazuko ya amri yako, na imetoa mng’ao wake juu ya ulimwengu wote, kulingana na yale yaliyoamriwa katika Vitabu vya Amri Yako.

Sifa iwe Kwako, Eee Mungu wangu, kwamba tumeamka kwenye wangavu wa nuru ya maarifa Yako. Tushushie basi, Ee Bwana wangu, kitakachotuwezesha kutomtaka yeyote ila Wewe, na kitakachotuondolea mshikamano wote kwa chochote ila Wewe. Andika, tena, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya wale walio wapendwa wangu, na kwa ajili ya jamaa zangu, mwanaume na mwanamke sawa, mema ya ulimwengu huu na ulimwengu ujao. Kisha utuweke salama, kupitia ulinzi Wako usioshindwa, Ee Wewe Uliyempendwa wa viumbe wote na Shauku ya malimwngu yote, kutokana na wale ambao Umewafanya kuwa wadhihirishaji wa mnong’onezaji muovu, ambaye hunong’ona katika vifua vya watu. Wewe una nguvu kufanya utakavyo. Wewe kweli, ndiye Mwenyezi Msaada katika Shida, Aliyepo Mwenyewe.

Mbariki, Ee Bwana Mungu wangu, Yeye Ambaye Umempa majina Yako bora kabisa, na ambaye kupitia kwake Wewe umewagawanya wamchao Mungu na waovu na utusaidie kwa rehema, tufanye Ulitakalo na Ulitamanilo. Wabariki, tena, Ee Mungu wangu, wao ambao ni Maneno Yako na Herufi Zako, na wale ambao wamekazia nyuso zao kuelekea Kwako, na kugeukia kwenye uso Wako na kuitika kwenye Mwito Wako.

Wewe hakika, ndiye Bwana na Mfalme wa watu wote na una nguvu juu ya vitu vyote.

#11208
- Bahá'u'lláh

 

ASUBUHI

Nimeamka katika himaya Yako, Ee Mungu wangu, na imembidi Yule ambaye anatafuta himaya hiyo kudumu ndani ya kimbilio la hifadhi Yako na Ngome ya Kinga Yako. Angaza moyo wangu, Ee Bwana wangu, kwa utukufu wa Mapambazuko ya Ufunuo Wako kama ulivyoangaza mwili wangu kwa mwangaza wa asubuhi wa fadhili Yako.

#11209
- Bahá'u'lláh

 

Nimeamka asubuhi hii kwa rehema Yako, Ee Mungu wangu, na nimeacha maskani yangu nikiwa na tumaini kamili Kwako, na nikijiweka katika uangalizi Wako. Nishushie basi, kutoka mbingu ya rehema Yako, baraka kutoka ubavuni Mwako, na Uniwezeshe kurudi maskani mwangu katika usalama kama Ulivyoniwezesha kuondoka nikiwa chini ya ulinzi Wako na mawazo yangu yakiwa yamekaziwa kabisa juu Yako.

Hakuna Mungu mwingine ila Wewe, Mmoja, Asiyelinganishwa, Ajuaye Yote, Mwenye hekima zote.

#11210
- Bahá'u'lláh

 

BAADHI YA SALA NYINGINE

Utukufu uwe Kwako Ee Mungu, kwa ajili ya Ufunuo wa Pendo lako kwa wanadamu! Ee Ewe Uliye Uzima na Mwanga wetu, ongoza watumishi Wako katika njia Yako, ututajirishe ndani Yako na kuwa huru kwa yote ila Wewe tu.

Ee Mungu, utufundishe umoja Wako na utupe utambuzi wa Umoja Wako ili tusione yeyote ila Wewe. Wewe u Mwenye Rehema na Mpaji wa Ukarimu!

Ee Mungu, washa katika mioyo ya wapendwa Wako moto wa upendo Wako ili uteketeze mawazo ya kila kitu ila Wewe.

Tufunulie, Ee Mungu, milele Yako iliyotukuka – kwamba Wewe umekuwako, na utakuwako, na kwamba hakuna Mungu mwingine ila Wewe tu. Hakika faraja na nguvu vinapatikana kwako.

#11223
- Bahá'u'lláh

 

Ee Mungu wangu! Ee Mungu wangu! Unganisha mioyo ya watumishi Wako na uwafunulie kusudi Lako lililo kuu. Wafuate amri Zako na kukaa katika sheria Yako Uwasaidie, Ee Mungu katika jitihada yao, na uwape nguvu kukutumikia. Ee Mungu, usiwaache peke yao bali uongoze hatua zao kwa mwanga wa maarifa yako na furahisha mioyo yao kwa upendo Wako. Hakika, Wewe ndiwe Msaidizi na Bwana Wao.

#11224
- Bahá'u'lláh

 

Sema: Ee Mungu, Mungu wangu! Vika kichwa changu kwa taji la haki na paji la uso wangu kwa pambo la uadilifu. Wewe, hakika, u Mwenye vipaji na baraka zote.

#11225
- Bahá'u'lláh

 

Ee, Mungu wangu! Nakuomba kwa Jina Lako tukufu kabisa, kunisaidia katika lile litakalofanya shughuli za watumishi Wako kufanikiwa, na miji Yako kusitawi. Wewe, kweli, una uwezo juu ya vitu vyote!

#11226
- Bahá'u'lláh

 

Mungu jalia kwamba nuru ya umoja iweze kufunika dunia yote, na kwamba mhuri, “Ufalme ni wa Mungu” uweze kupigwa juu ya paji la uso la watu wake wote.

#11227
- Bahá'u'lláh

 

Kuna mwondoa shida yeyote isipokuwa Mungu? Sema: Mungu asifiwe! Yeye ni Mungu! Wote ni watumishi Wake, na wote wanaishi kwa mapenzi Yake!

#11228
- The Báb

 

Ee Mungu, changamsha na uifurahishe roho yangu. Takasa moyo wangu. Ng’arisha fikira zangu. Naacha shughuli zangu zote mikononi Mwako. Wewe U kiongozi na kimbilio langu.. Sitakuwa na majuto wala kuhuzunika tena, nitafurahi na kuchangamka. Ee Mungu! Sitajawa na mashaka tena, wala sitaacha taabu zinisumbue tena. Sitaishi kwa vitu visivyofaa maishani.

Ee Mungu! Wewe U rafiki kwangu zaidi ya mimi nilivyo mweneyewe kwangu. Najitoa mwenyewe Kwako, Ee Bwana.

#11229
- `Abdu'l-Bahá

 

Ee Bwana wangu, Mpendwa wangu, Haja yangu! Nifanye rafiki katika ukiwa wangu na ufuatane nami katika uhamisho wangu. Ondoa huzuni yangu. Nifanye kujitoa kwa uzuri Wako. Nitoe kwa vyote ila Wewe. Nivutie kupitia manukato Yako ya utakatifu. Nifanye kuwa mshirika katika Ufalme Wako na wale ambao wamejitenga na yote isipokuwa Wewe na wanaotamani kuhudumu katika enzi yako takatifu na wanaosimama kufanya kazi katika Hoja Yako. Uniwezeshe kuwa mmoja wa watumishi wako wa kike ambao wamepata ridhaa Yako njema. Hakika, Wewe ni mwenye Rehema, Karimu.

#11230
- `Abdu'l-Bahá

 

Ee Bwana Mungu wangu! Wasaidie wapendwa Wako kuwa imara katika Imani Yako, kutembea katika njia Zako, kuwa dhabiti katika Hoja Yako. Wape neema Yako kuzuia mashambulio ya nafsi na tamaa, kufuata mwanga wa Uongozi Mtakatifu. Wewe ni Mwenye nguvu, Mwenye rehema, Aishiye Mwenyewe, Mpaji, Mwenye huruma, Mwenyezi, Karibu) kabisa.

#11231
- `Abdu'l-Bahá

 

Bwana, sisi tu watu wa kuhurumiwa, utupe kibali Chako; tu maskini, utupe fungu kutoka kwa wingi wa ukwasi Wako; tu wenye haja, ututosheleze; tumetahayarishwa, utupe neema Yako. Ndege wa anga na wanyama wa konde wapokea chakula chao kutoka Kwako kila siku na viumbe wote wana ulinzi na upendo Wako.

Usimnyime mnyonge huyu neema Yako ya ajabu na uijalie nafsi hii dhaifu Baraka Yako kwa nguvu zako.

Utupe hakula chetu cha kila siku na utuongezee maisha yetu, ili tusitegemee yeyote ila Wewe, tuzungumze nawe, tutembee katika njia Zako na kutangaza mafumbo Yako. Wewe u Mwenyezi na Mwenye upendo na Mpaji wa wanadamu.

#11232
- `Abdu'l-Bahá

 

Ee Bwana! Sisi tu wanyonge; tuimarishe. Ee Mungu! Tu wajinga; tufanye wajuzi. Ee Bwana! Tu maskini; tufanye matajiri. Ee Mungu! Tu wafu; tuhuishe. Ee Bwana! Sisi tu fedheha yenyewe; tutukuze katika Ufalme Wako. Ukitusaidia, Ee Bwana, tutakuwa kama nyota zimemetekazo. Usipotusaidia, tutakuwa na hali ya chini kuliko udongo. Ee Bwana! Tuimarishe. Ee Mungu! Tujalie ushindi. Ee Mungu! Tuwezeshe kushinda nafsi na tamaa Ee Bwana! Tuokoe kutoka katika utumwa wa mambo ya kidunia. Ee Bwana! Tuhuishe kupitia pumzi ya Roho Mtakatifu ili tuamke kukutumikia, tujishughulishe katika kukuabudu Wewe na kujibidiisha wenyewe katika ufalme Wako kwa ukweli kabisa. Ee Bwana! U Mwenye nguvu! Ee Mungu, U Msamehevu! Ee Bwana, U Mwenye Rehema!

#11233
- `Abdu'l-Bahá

 

Ee Mungu, Mungu wangu! Wakinge watumishi Wako waaminifu na maovu ya tamaa walinde na jicho Lako la upendo dhidi ya chuki, karaha ni kijicho, uwahifadhi katika Neno Lako lisilopotoka wawe salama kwa mishale ya mashaka, wafanye wajumbe wa ishara Zako tukufu, ng’arisha nyuso zao kwa miale inayong’aa itokayo katika chimbuko la umoja Wako mtukufu, furahisha mioyo yao kwa maneno yatokayo katika ufalme Wako mtukufu na tia nguvu viuno vyao kwa nguvu itokayo katika milki Yako tukufu. Wewe ni Mwenye Baraka Zote Mlinzi, Mwenyezi na Mwenye rehema.

#11234
- `Abdu'l-Bahá

 

Ewe Mungu! Ewe Mungu! Huyu ni ndege aliyevunjika mabawa yake na kuruka kwake ni shida sana. Msaidie ili kwamba aweze kuruka kwa upeo wa ufanisi na wokovu, wekelea kuruka kwake kwa furaha kuu na upendo katika nafasi isiyo na kikomo, inua sauti yake katika Jina Lako tukufu ndani ya sehemu zote, changamsha masikio na mwito huu, na ng’arisha macho kwa kutazama dalili za maongozi!

Ewe Bwana! Mimi ni pweke, mmoja na aliye chini. Kwangu mimi sina wa kutegemea ila Wewe, sina wa kunisaidia isipokuwa Wewe na sina wa kunihifadhi kando Yako. Nithibitishe katika kazi yangu, nisaidie na majeshi ya malaika Wako, nifanye mshindi katika kuendeleza neno Lako na uniwezeshe kunena kutoka kwa hekima Yako juu ya viumbe Wako. Hakika Wewe U Mtunza maskini na Mtetezi wa walio wadogo na kweli U Mwenye nguvu, Mwenye uwezo na Asiyeshurutishwa!

#11235
- `Abdu'l-Bahá

 

BARAZA LA KIROHO

Wakati wowote muingiapo chumba cha mashauriano semeni sala hii kwa moyo upumao na mapenzi ya Mungu na ulimi uliotakasika kutokana na vyote ila kumbukumbu Yake, ili kwamba Mwenye-uwezo wote aweze kwa neema kuwasaidia kupata ushindi mkuu:

Ee Mungu, Mungu wangu! Sisi tu watumishi Wako ambao wameugeukia kwa moyo uso Wako mtakatifu, ambao wamejitenga wenyewe kutokana na vyote kando Yako katika Siku hii tukufu. Tumekusanyika katika Baraza hili la Kiroho, tukiunganika katika maoni na mawazo yetu, na malengo yetu yakioanishwa kulitukuza Neno Lako kati ya wanadamu. Ee Bwana, Mungu wetu! Tufanye ishara za uongozi Wako mtakatifu, bendera za Imani Yako iliyotukuka kati ya watu, watumishi kwenye Ahadi Yako kuu, Ewe Bwana wetu Uliye Juu kabisa, wadhihirishaji wa Umoja Wako Mtakatifu katika Ufalme Wako wa Abha, na nyota angavu ziangazazo juu ya sehemu zote. Bwana! Tusaidie kuwa bahari zisukasukazo kwa mawimbi ya neema Yako ya ajabu, mito itiririkayo kutoka vilele Vyako vilivyotukuka kabisa, matunda mema juu ya mti wa Imani Yako ya mbinguni, miti ipepeayo kwa pepo za Baraka Yako katika shamba Lako la mizabibu la mbinguni. Ee Mungu! Zifanye roho zetu zitegemee Aya za Umoja Wako Mtakatifu, mioyo yetu ikichangamshwa na mmiminiko wa neema Yako, ili tuweze kuunganika hata kama mawimbi ya bahari moja na kuunganishwa pamoja kama miale ya nuru Yako ing’aayo; ili mawazo yetu, maoni yetu, yaweze kuwa kama uhalisia mmoja ukidhihirisha roho ya umoja ulimwenguni mwote. Wewe ni Mwenye neema, Karimu, Mpaji, Mweza yote, Mwenye rehema, Mwenye huruma.

#11215
- `Abdu'l-Bahá

 

JIONI

Ee Mungu wangu, Bwana wangu, Lengo la shauku yangu! Mtumishi wako huyu, atazamia kusinzia katika kivuli cha rehema Yako na kupumzika chini ya chandalua cha rehema Yako, akiomba uangalizi Wako na ulinzi Wako.

Ninakuomba, Ee Bwana wangu, kwa jicho Lako ambalo halisinzii, kuyalinda macho yangu yasitazame mwingine kando Yako. Imarisha, basi, kuona kwayo ili yaweze kutambua ishara Zako, na kutazama Upeo wa Ufunuo Wako. Wewe ndiye Yule Ambaye mbele ya ufunuo wa ukuu Wake kipeo cha nguvu kimetetemeka.

Hayupo Mungu ila Wewe, Mwenyezi, mtiisha kabisa, Asiyeshurutishwa.

#11211
- Bahá'u'lláh

 

KUPONYA

Jina Lako ndilo kuponywa kwangu, Ee Mungu wangu, na kukukumbuka Wewe ni dawa yangu. Kuwa karibu na Wewe ndilo tumaini langu na upendo Kwako ndio mwenzi Wangu. Huruma Yako kwangu ni kiponyesho changu na msaada kwangu katika ulimwengu huu na ulimwengu ujao. Wewe, hakika ni Mwenye Baraka Zote, Ajuaye yote, Mwenye Hekima zote.

#11214
- Bahá'u'lláh

 

MCHANGO KWENYE AKIBA

Marafiki wote wa Mungu . . . lazima wachangie kwa uwezo wao wote, hata mchango wao uwe mdogo kiasi gani. Mungu haitwishi mzigo roho kupita uwezo wake. Michango kama hiyo ni lazima itoke kwa vituo vyote na waamini. Enyi marafiki wa Mungu! Muwe na hakika kwamba badala ya michango hii, kilimo chenu, viwanda vyenu, na biashara zenu vitabarikiwa kwa nyongeza nyingi, kwa thawabu nzuri na Baraka. Yule ajaye na kitendo kimoja kizuri, atapata thawabu mara kumi. Hakuna shaka kwamba Bwana Aliye hai Atawathibitisha kwa wingi wale wanaotumia mali yao katika njia Yake.

Ee Mungu, Mungu wangu! Ng’arisha nyuso za wapenzi Wako wa kweli na uwafariji kwa majeshi ya malaika wa ushindi. Ikaze miguu yao kwenye njia Yako iliyonyooka na kutoka kwenye Baraka Yako ya zamani, ufungulie mbele yao milango ya neema Zako; kwani wanatumia njiani Mwako kile Ulichowapa wakilinda Imani Yako, wakiweka tumaini lao katika kumbukumbu Yako, wakitoa mioyo yao kwa ajili ya upendo Wako na bila kuzuia walichonacho katika kusujudu kwa Uzuri Wako na katika kutafuta njia za kukupendeza.

Ee Bwan wangu! Amuru kwa ajili yao fungu tele, tuzo lililokusudiwa) na zawadi ya uhakika.

Hakika Wewe ndiye Mhifadhi, Msaidizi, Karimu, Mwenye Baraka, Mpaji daima.

#11220
- `Abdu'l-Bahá

 

MFUNGO

Sifa iwe Kwako, Ee Bwana Mungu wangu! Nakusihi Wewe kwa Ufunuo huu ambao kwao giza limegeuzwa katika mwangaza, kupitia kwake Hekalu liendewalo mara kwa mara limejengwa, na Waraka Ulioandikwa umefunuliwa, na Gombo Lililoenea likafunuliwa, kunitumia mimi pamoja na wao walio wenzangu yale ambayo yatatuwezesha kupaa katika mbingu za utukufu Wako bora kabisa, na yatatutakasa kutokana na madoa ya mashaka kama yale ambayo yamewazuia wasio wanyoofu wasiingie katika hema la umoja Wako.

Mimi ndiye, Ee Bwana wangu, ambaye ameshikilia kwa uthabiti kamba ya wema Wako wa upendo, na nimeshikamana na upindo wa neema na hisani Zako. Niagizie mimi na wale niwapendao, mema ya ulimwengu huu na ulimwengu ujao. Uwape basi, kipaji kilichofichwa ulichoamuru kwa wateule kati ya viumbe Wako.

Hizi ndizo siku, Ee Bwana wangu, ambamo umewaamuru watumishi Wako kuadhimisha mfungo. Amebarikiwa Yule ambaye anaadhimisha mfungo kwa ajili Yako hasa na akiwa amejitenga kabisa na mambo yote ila Wewe. Nisaide mimi na uwasaidie wao, Ee Bwana wangu, kukutii wewe na kushika amri Zako. Wewe, hakika, una uwezo kufanya lolote uchagualo.

Hakuna Mungu ila Wewe, Ajuaye yote, Mwenye hekima zote. Sifa zote ziwe kwa Mungu, Bwana wa malimwengu yote.

#11212
- Bahá'u'lláh

 

NDOA

Utukufu uwe Kwako, Ee Mungu wangu! Hakika mtumishi Wako huyu na mjakazi Wako huyu wamejikusanya chini ya kivuli cha rehema Yako na wameunganika kwa fadhili na ukarimu Wako. Ee Bwana! Wasaidie katika dunia Yako hii na Ufalme Wako na uwachagulie kila jema kupitia Baraka Yako na rehema. Ee Bwana! Wathibitishe katika utumishi Wako na uwasaidie katika huduma Yako. Waache wawe ishara za Jina Lako ulimwenguni Mwako na uwalinde kupitia vipaji Vyako visivyokwisha katika ulimwengu huu na ulimwengu ujao. Ee Bwana! Wanasujudu mbele ya Ufalme wa neema Yako wakiomba mbele ya milki ya umoja Wako. Hakika wameoana katika utiifu kwa amri Yako. Wafanye wawe ishara za utulivu na umoja mpaka mwisho. Hakika Wewe ni Mweza yote, Aliyeko pote, Mwenyezi

#11213
- `Abdu'l-Bahá

 

SALA KWA WALIOKUFA

Ee Mungu wangu! Huyu ni mtumishi Wako na mwana wa mtumishi Wako ambaye amekuamini Wewe na ishara Zako, na kuelekeza uso wake Kwako, amejitenga kabisa kutoka kwa vyote ila Wewe. Wewe hakika, ndiwe wa wale ambao huonyesha rehema, mwenye rehema kabisa.

Mtendee, Ee Ewe Ambaye husamehe dhambi za watu na kusetiri kasoro zao, kama istahilivyo mbingu ya Baraka Yako na bahari ya rehema Yako. Mjalie kuingia katika mipaka ya rehema Yako bora kabisa ambayo ilikuwapo kabla ya kuanzishwa kwa dunia na mbingu. Hakuna Mungu ila Wewe, Asameheaye daima, Karimu Kabisa.

Ndiposa tena, arudie mara sita maamkuzi “Alláh’u’Abhá”, na tena arudie mara kumi na tisa kila moja ya aya zifuatazo:

Sisi sote, hakika, twamwabudu Mungu.

Sisi sote, hakika twasujudu mbele ya Mungu.

Sisi sote, hakika tumejitoa kwa Mungu.

Sisi sote, hakika, twamsifu Mungu.

Sisi sote, hakika, twatoa shukrani kwa Mungu.

Sisi sote, hakika, tu wenye subira katika Mungu.

(Ikiwa marehemu ni mwanamke, hebu aseme: Huyu ni mtumishi Wako wa kike na binti wa mtumishi Wako wa kike, n.k. . . . )

#11221
- Bahá'u'lláh

 

Ee Mungu wangu! Ee Ewe msamehe dhambi, Mpaji thawabu, mwondoa huzuni!

Hakika, nakusihi kusamehe dhambi za wale walioacha vazi la kimwili na wamepaa kwenye ulimwengu wa kiroho.

Ee Bwana wangu! Uwatakase kutokana na makosa, ondoa huzuni zao, na ubadilshe giza lao katika mwanga. Wafanye waingie bustani ya furaha, uwatakase kwa maji safi kabisa, na uwajalie waone utukufu Wako kwenye mlima ulio bora kabisa.

#11222
- `Abdu'l-Bahá

 

SALA KWA WATOTO NA VIJANA

Ee Mungu! Mlee mtoto huyu mchanga katika moyo wa upendo Wako, na umpe maziwa kutoka katika kifua cha Majaliwa Yako. Palilia mche huu mchanga katika bustani ya waridi ya upendo Wako na umsaidie kukua kupitia manyunyu ya baraka Yako. Mfanye mtoto wa Ufalme na umuongoze kwenye milki Yako ya mbinguni. Wewe U mwenye nguvu na mwema, na Wewe U Mpaji, Karimu, Bwana wa Baraka zisizo kifani.

#11216
- `Abdu'l-Bahá

 

Ee Mungu! Wafundishe watoto hawa. Watoto hawa ni miche ya kiunga Chako cha miti ya matunda, maua ya shamba Lako, waridi ya bustani Yako. Acha mvua Yako iwanyeshee; acha Jua la ukweli liwaangazie na upendo Wako. Acha upendo Wako uwaburudishe ili kwamba waweze kufundishwa, kukua na kuendelea na kuonekana katika uzuri wa juu kabisa. Wewe u Mpaji! Wewe u Mwenye huruma.

#11217
- `Abdu'l-Bahá

 

Ee Bwana! Mfanye kijana huyu mwangavu na ujalie Baraka Yako juu ya kiumbe huyu mnyonge. Umpe hekima, umjalie nguvu zaidi kwenye kila mapambazuko na umkinge katika kivuli cha ulinzi Wako ili aweze kuondolewa katika makosa, aweze kujiweka katika huduma ya Hoja Yako, aweze kuwaongoza wapotovu, awaachilie mateka na kuwaamsha wazembe, ili wote waweze kubarikiwa kwa kumbukumbu na sifa Yako.

Wewe ndiye Mwenye uwezo na Mwenye nguvu.

#11218
- `Abdu'l-Bahá

 

Ee Mungu, niongoze, nilinde, nifanye taa inayowaka na nyota ing’aayo. Wewe ni Mwenyezi na Mwenye nguvu.

#11219
- `Abdu'l-Bahá

 

Occasional

Tablets