The Universal House of Justice
Ridván 2022
To the Bahá’ís of the World
Dearly loved Friends,
Mwaka wa maandalizi na tafakari, hali kadhalika wa juhudi kubwa, umehitimishwa, ukipambanuliwa kwa jitihada za marafiki kote ulimwenguni kuashiria miaka mia moja ya Kupaa kwa ‘Abdu’l-Bahá, zikijumuisha utumaji wa wawakilishi kushiriki katika tukio maalum la kumuenzi Yeye katika Nchi Takatifu. Kupitia jitihada hizi, uvuvio uliotolewa na maisha ya ‘Abdu’l-Bahá umehisiwa na roho zisizo na idadi na si tu Wabahá’í. Kumjali Kwake kila mwana-familia wa jamii ya wanadamu, kazi Yake ya ufundishaji, uendelezaji Wake wa shughuli za elimu na usitawi wa kijamii, michango Yake ya kina kwenye mijadala kote Magharibi na Mashariki, utiaji Wake moyo wa dhati wa miradi ya kujenga Nyumba za Ibada, uundaji Wake wa mwanzoni wa miundo ya utawala wa Kibahá’í, ukuzaji Wake wa sura mbalimbali za maisha ya jumuiya—sura zote hizi zinazoshamirishana za maisha Yake zilikuwa taswira za kujitoa Kwake kwa daima na kikamilifu kwenye kumtumikia Mungu na kuitumikia jamii ya wanadamu. Mbali na kuwa kinara wa kutegemewa wa mamlaka ya kimaadili na umaizi wa kiroho wa hali ya juu, ‘Abdu’l-Bahá alikuwa njia isiyo na doa ambayo kwayo nguvu zilizoachiliwa na Ufunuo wa Bahá’u’lláh zingeweza kutenda kazi juu ya ulimwengu. Ili kutambua nguvu ya ujengaji jamii ambayo Imani inayo, mtu hahitaji kuangalia mbali zaidi kuliko mafanikio ya ‘Abdu’l-Bahá wakati wa utumishi Wake na matokeo yabadilishayo ya miongozo iliyotiririka bila kukoma kutoka kwenye kalamu Yake. Maendeleo mengi sana ya kushangaza yaliyofanywa na jumuiya ya Kibahá’í ya sasa--ambayo yalitazamwa katika ujumbe wetu kwenu wa Riḍván iliyopita—hufuatilia vyanzo vyake kwenye vitendo, maamuzi na maelekezo ya ‘Abdu’l-Bahá.
Ni ya kufaa namna gani, basi, kwamba shukrani za pamoja za jumuiya ya Kibahá’í kwa Mfano wake mkamilifu inavyopaswa kuunda mwanzo wa uanzishwaji wake wa shughuli kuu ikimakinikia juu ya uachiliaji wa nguvu ya Imani ya ujengaji jamii kwa viwango vikubwa zaidi. Maeneo ya jitihada ambayo huangukia ndani ya uwanda wa Mpango wa Miaka Tisa, na wa mfululizo wa sasa wa Mipango, inaelekezwa kwenye utimizaji wa shabaha hii kuu. Pia ni shabaha ya zaidi ya makongamano 10,000 yanayofanyika kote duniani kuashiria uzinduzi wa shughuli hii kuu ya kiroho. Makongamano haya, yanayotarajiwa kukaribisha idadi isiyo na mfano ya washiriki, siyo tu yawaleta pamoja Wabahá’í bali pia watakia heri wengine wengi wa jamii ya wanadamu ambao hushiriki nao shauku ya kukuza umoja na kuboresha ulimwengu. Dhamira yao na hisia yao thabiti ya kusudi vinaakisiwa katika moyo uliofanyizwa kwenye mikusanyiko ambayo tayari imekwishatokea, ambapo washiriki wameamshwa sana kwa ushauriano wenye nguvu ambao wamechangia kwa muono wa pamoja uliochunguzwa kwenye matukio haya ya shangwe. Tunatazama kwa matarajio makubwa kwa yale ambayo miezi na miaka ijayo itayaleta.
Tangu tulipotoa ujumbe wetu wa 30 Desemba 2021 kwa Kongamano la Washauri, Mabaraza ya Kiroho ya Kitaifa na Halmashauri za Kibaha’i za Kanda yamekuwa yakitathmini kwa shauku uwezekano wa kushadidisha mchakato wa ukuaji katika klasta zilizo ndani ya maeneo yao ya mamlaka katika kipindi cha Mpango wa Miaka Tisa. Tunahisi ingekuwa ya kufaa, kwa kusudi la kupima maendeleo yaliyofanyika kwa kipindi hicho, kuuona Mpango huu kama unaojikunjua katika awamu mbili za kipindi cha miaka minne na mitano, na Mabaraza ya Kitaifa yalialikwa kufikiria maendeleo wanayoyatarajia kuyaona katika jumuiya zao husika ifikapo Riḍván 2026 na kisha ifikapo Riḍván 2031. Zoezi hili pia lilihusisha kutathminiwa upya kwa mipaka ya klasta, na matokeo ya marekebisho haya ni kwamba jumla ya idadi ya klasta ulimwenguni imepanda kwa robo na sasa ipo zaidi ya 22,000. Kwa kutegemea matabiri yaliyopokelewa, inakadiriwa kwamba, ifikapo mwisho wa Mpango, programu za ukuaji kwa kiwango fulani cha maendeleo zitakuwepo katika takribani klasta 14,000 kati ya hizi. Kutoka miongoni mwa hizo, idadi ambazo programu ya ukuaji ingeweza kufikiriwa kuwa shadidi inakisiwa kupanda hadi kufikia 11,000 katika kipindi hicho hicho. Na kati ya hizi, inatazamiwa kwamba idadi ya klasta ambamo hatua ya tatu ya ukuaji itakuwa imevukwa itapanda zaidi ya 5,000 ifikapo 2031. Pasipo swali, ili kupiga hatua kama hizo zitahitajika jitihada kubwa mno kwa kipindi chote cha Mpango. Bado tunaona haya kuwa ni matarajio ya kupambania, kwani yanawakilisha tathmini yenye nia kuu lakini ya dhati ya kile kilicho ndani ya uwezo wa kufikiwa.
Hiki ndicho kinachosemwa. Shabaha kama hizo zisingeweza kufikiriwa kiuhalisia kama asasi za kiutawala na mawakala zisingekuwa zimekua dhahiri, kuzijalia uwezo utambulikao uliokuzwa kusimamia mambo ya jumuiya ambazo shughuli zake zimeongezeka kwa haraka, zikikumbatia idadi kubwa na ikuayo ya roho ndugu. Isingewezekana kutarajia ukuaji wa namna hiyo kama shauku ya kujifunza—kutenda, kutafakari, kuchota umaizi na kufyonza umaizi unaoibuka kwingineko—isingekuwa imekuzwa kwenye ngazi zote, kufikia kwenye ngazi ya umma ya jumuiya. Na jitihada imaanishwayo kwa makadirio kama hayo isingewezekana kama mbinu za kimpangilio kwenye kazi ya ufundishaji na kwenye ukuzaji wa rasilimali watu isingekuwa imeendelea kuwa dhahiri katika ulimwengu wa Kibahá’í. Yote hii imeleta ongezeko la utambuzi katika jumuiya ya Kibahá’í wa utambulisho na kusudi lake. Dhamira ya kuwa na mtazamo wa nje katika mchakato wa ujengaji jumuiya tayari ilishakuwa sehemu madhunuti ya utamaduni katika maeneo mengi, mengi; sasa imeshamiri, katika idadi iongezekayo ya jumuiya, katika hisia ya jukumu halisi kwa ajili ya maendeleo ya kiroho na ya kimwili ya makundi makubwa na makubwa zaidi katika jamii, mbali zaidi ya uumini wa jumuiya ya Kibahá’í yenyewe. Jitihada za marafiki kujenga jumuiya, kujihusisha katika shughuli za kijamii, na kuchangia kwenye mijadala inayoendelea ya jamii zimeunganika katika shughuli moja ya kiulimwengu, zikifungamana kwa pamoja kwa muundo wa pamoja wa utendaji, ukilenga juu ya kusaidia jamii ya wanadamu kuanzisha mambo yake juu ya msingi wa kanuni za kiroho.
Umuhimu wa maendeleo tuliyokwishayaelezea, kufikia hatua hii miaka mia moja baada ya uzinduzi wa Utaratibu wa Utawala, hauwezi kupuuzwa. Katika ongezeko lisilo la kawaida la uwezo lililotokea katika miongo miwili iliyopita—na ambao umewezesha ulimwengu wa Kibahá’í kutazama jitihada zake kwa maana ya uachiliaji wa nguvu ya Imani ya ujengaji jamii—tunaona ushahidi usiopingika kwamba Hoja ya Mungu imeingia kipindi cha sita cha Zama yake ya Ujenzi. Riḍván iliyopita tulitangaza kwamba hali iliyoenea ya idadi kubwa inayoshiriki katika shughuli za Kibahá’í, ikiwashwa kwa imani, na ikijitwalia ujuzi na uwezo mwingi kuhudumia jumuiya zao iliashiria kwamba kipindi cha tatu cha Mpango Mtakatifu wa Bwana kilikuwa kimeanza; hivyo, Mpango wa Mwaka Mmoja, kwenye mwanzo wake wakati ule na kwenye hitimisho lake sasa, umekuja kuashiria maendeleo kadhaa ya kihistoria yaliyofanywa na kundi la waaminifu. Na kwenye kizingiti cha shughuli kuu mpya, shirika hili lililounganika la waumini lipo tayari kutwaa fursa zilizo wazi mbele yake.
Sura inayojitokeza ya kipindi kinachomalizika sasa ilikuwa ni ujenzi wa Nyumba za mwisho za Ibada za kibara na uanzishwaji wa miradi ya kujenga Nyumba za Ibada kwenye ngazi za kitaifa na mahali. Mafunzo mengi yamepatikana, na Wabahá’í kote ulimwenguni, kuhusu dhana ya Mashriqu’l-Adhkár na muunganiko wa ibada na huduma inavyovijumuisha. Wakati wa kipindi cha sita cha Zama ya Ujenzi, mengi zaidi yatapatikana kuhusu njia ambayo huongoza kutoka maendeleo ndani ya jumuiya yenye maisha ya ibada yanayoshamiri—na huduma ambayo huivuvia—hadi utokezaji wa Mashriqu’l-Adhkár. Mashauriano yanaanza na baadhi ya Mabaraza ya Kiroho ya Kitaifa, na haya yakiendelea, tutawatangazia kila baada ya kipindi fulani mahali ambako Nyumba za Ibada za Kibahá’í zitajengwa katika miaka ijayo.
Furaha yetu ya kuona jumuiya ya Jina Kuu Kabisa ikienda kutoka nguvu hadi nguvu inapunguzwa na huzuni yetu kuu ya kuona ung’ang’anifu wa hali na mafarakano ulimwenguni ambavyo husababisha mateso yenye taabu na kutokuwa na matumaini—hususan, kuona kurudia kwa nguvu za uharibifu ambazo zimevuruga mambo ya kimataifa wakati zikipeleka vitisho kwa watu. Tunafahamu fika na tunahakikishiwa tena kwamba, kama jumuiya za Kibahá’í mara kwa mara tumeonesha katika miktadha mingi mbalimbali, wafuasi wa Bahá’u’lláh wamejidhatiti katika kuleta ahueni na msaada kwa wale wanaowazunguka, bila kujali hali zao ni za dhiki kiasi gani. Lakini mpaka pale jamii ya wanadamu kwa jumla itakapoamua kuweka mambo yake juu ya misingi ya haki na kweli, ole, imetabiriwa kuwa na misukosuko kutoka hali moja ya hatari hadi nyingine. Tunasali kwamba, ikiwa mlipuko wa sasa wa vita huko Ulaya utatoa mafunzo yoyote kwa ajili ya siku zijazo, itakuwa kama kumbusho la haraka la muelekeo ambao ulimwengu lazima uchukue kama unataka kufikia amani ya kweli na ya kudumu. Kanuni zilizotolewa na Bahá’u’lláh kwa tawala na marais wa kipindi Chake, na majukumu mazito ambayo Yeye aliagiza kwa watawala wa wakati uliopita na sasa, huenda yanafaa zaidi na ya muhimu leo kuliko yalipoandikwa kwa mara ya kwanza kwa Kalamu Yake. Kwa Wabahá’í, maendeleo yasiyozuilika ya Mpango Mkuu wa Mungu—ukiambatana na mateso na misukosuko, lakini hatimaye ukiisukuma jamii ya wanadamu kuelekea kwenye haki, amani na umoja—ni muktadha ambao ndani yake Mpango Mdogo wa Mungu, ambao waumini kwa kiasi kikubwa ndiyo wanaoshughulika nao, hukunjuka. Hali mbaya ya kiutendaji ya jamii ya sasa hufanya hitaji la uachilia nguvu ya Imani ya ujengaji jamii kuwa wazi kwa kiwango kikubwa na ya lazima. Hatuwezi bali kutegemea kwamba, kwa sasa machafuko na fujo vitaendelea kuutesa ulimwengu; bila shaka mtatambua, hivyo, kwa nini kila ombi la dhati tunalolitoa kwa ajili ya watoto wote wa Mungu kuachiliwa kutoka fadhaa na dhiki kali linaunganishwa sawia na sala ya dhati kwa ajili ya mafanikio ya huduma ihitajikayo sana mnayoitoa kwa ajil ya Hoja ya Mwana-Mfalme wa Amani.
Katika kila klasta ambako shughuli za Mpango zinapata msukumo, tunaona maendeleo ya jumuiya zenye tabia bora tulizozielezea katika ujumbe wa 30 Desemba 2021. Wakati jamii zikipitia mifadhaiko ya aina mbalimbali, wafuasi wa Uzuri wa Abhá lazima wajipambanue zaidi na zaidi kwa sifa zao za unyumbulikaji na urazini, kwa kiwango chao cha mwenendo na ushikiliaji wao wa kanuni, na kwa huruma, kujitenga na ustahimilifu wanazozionesha katika ufuatiliaji wao wa umoja. Mara kwa mara, tabia na mielekeo bainifu ioneshwayo na waumini katika nyakati za shida kali zimewasukuma watu kuwageukia Wabahá’í kwa ajili ya maelezo, ushauri na msaada, hasa pale maisha ya jamii yanapovurugwa na kukabiliwa na taabu na vikwazo visivyotabirika. Katika kushiriki chunguzi hizi, tunatambua kwamba jumuiya ya Kibahá’í yenyewe pia inapitia madhara ya nguvu za uchangukaji zilizo kazini katika ulimwengu. Zaidi, tunatambua kwamba kadiri jitihada za marafiki za kutangaza Neno la Mungu zilivyo kuu zaidi, ndivyo nguvu za ukinzani watakazokutana nazo zitakavyokuwa na nguvu zaidi, punde au baadaye, kutoka maeneo mbalimbali. Sharti waimarishe roho zao dhidi ya majaribu ambayo kwa hakika yatakuja, haya yasije yakatatiza uadilifu wa jitihada zao. Lakini waumini wanafahamu fika kwamba dhoruba zozote zilizo mbele yao, safina ya Hoja ni sawa kwao wote. Hatua zinazofuatana za safari yake zimeshaviona vidokezo vya hali ya hewa na wanakwea juu ya mawimbi. Sasa inaelekea kwenye upeo mpya. Mathibitisho ya Mwenyezi ndiyo dhoruba zinazojaza matanga yake na kuisukuma kuelekea mwisho wa safari yake. Na Agano ndiyo nyota yake iiongozayo, ikikiweka chombo kitakatifu kielekee kwenye uelekeo wake wa uhakika na yakini. Acha wakazi wa mbinguni watume baraka juu ya wote wasafirio ndai yake.
- The Universal House of Justice